HAKI ZA UTANGAZAJI: JINSI TULIWEZA KUSHUHUDIA MICHEZO YA OLIMPIKI TUKIWA KENYA

HAKI ZA UTANGAZAJI: JINSI TULIWEZA KUSHUHUDIA MICHEZO YA OLIMPIKI TUKIWA KENYA

Utangulizi

Duniani, Eliud Kipchoge anajulikana kama mwanaridha hodari, haswa katika mbio za marathoni. Kwa sasa, anashikilia rekodi rasmi ya dunia ya masaa 2:01:39 katika mbio za marathoni. Kipchoge pia ni mshindi wa dhahabu katika mbio za marathoni za Olimpiki. Mwaka huu, katika Michezo ya Olimpiki kule Tokyo, Japan, Kipchoge aliweza kushinda na kuhifadhi dhahabu yake. Ushindi huu ulimfanya kuwa mmoja kati ya wakimbiaji watatu kushinda medali mbili za dhahabu, moja baada ya nyingine, katika mbio za marathoni za wanaume za Olimpiki.Wakenya na mashabiki walikesha usiku kucha ili kufuatilia mbio hizo kwa runinga zao1 na kushuhudia ushindi wa Kipchoge.

Michezo kama vile ya Olimpiki, Mashindano ya Soka ya UEFA, Formula 1 na kadhalika hutazamwa na kufuatiliwa ulimwenguni kote na mashabiki wengi. Watu wenye asili tofauti hukusanyika pamoja ili kuburidishwa na kushuhudia michezo hizi. Burudani hizi zimewezeshwa na ubunifu wa utangazaji wa moja kwa moja kutoka uwanjani hadi kwa runinga za mashabiki.

Lengo la maandishi haya ni kujadili haki zinazohusika katika utangazaji wa moja kwa moja wa michezo (live broadcast) na haki zinazoruhusu vituo vya habari vya nchi mbalimbali kutangaza michezo hizo (broadcasts).

Haki za Utangazaji

Haki za utangazaji ni moja wapo ya haki zilizopo katika familia ya Haki Miliki (Intellectual Property Rights). Haswa, haki hizi huhusiana na haki zinazolinda sanaa (Copyrights).

Haki za utangazaji hulinda usambazaji wa sauti au picha zilizo na sauti, kwa watu wa umma kwa njia zisizo na waya; iwe kwa kupitia redio, runinga au setilaiti. Haki hizi hutuzwa mashirika ya utangazaji na huwapa uwezo wa kuidhinisha au kukataza utangazaji, na uchapishaji wa matangazo yao na watu au mashirika mengine ya utangazaji.

Haki hizi hulinda jinsi mashirika ya utangazaji huunda programu zao kwenye siginali za utangazaji, na pia hulinda uwasilishaji wa programu hizo kwa watazamaji. Lengo kuu la haki hizi ni kutuza pembejeo za mashirika ya utangazaji za kiuchumi na ubunifu.

Kama nilivyo angazia hapo awali, haki hizi mara nyingi hutuzwa kwa mashirika ya utangazaji na kuwapa umiliki wa kipekee juu ya kazi zao zilizoundwa kwa ajili ya kuwasilishwa kwa watazamaji. Umiliki wa haki hizi humpa mwenye haki uwezo wa kuzuia watu na mashirika mengine kutumia kazi zake bila leseni au ruhusa yake.

Matumizi ya, na Utekelezaji wa Haki za Utangazaji

Kulingana na Shirika la Haki Miliki Duniani (World Intellectual Property Organization -WIPO2), haki za utangazaji zina malengo matatu makuu;

  1. Kulinda uwekezajiwa gharama kubwa inayohitajika ili kupeperusha habari hewani.

  2. Kutambua na kutuza juhudi za ujasiriamali za mashirika ya utangazaji.

  3. Kutambua na kutuza mchango wa mashirika ya utangazaji katika uenezaji wa habari na utamaduni.

Hivyo basi, tukizingatia malengo haya, na kama nilivyoashiria hapo awali, haki za utangazaji huwapa wamiliki wake uwezo wakuamua jinsi kazi zao zitasambazwa na kuchapishwa. Uwezo huu huwapa mamlaka na haki ya kuidhinisha au kuzuia utangazaji, na uchapishaji wa matangazo yao na watu au mashirika mengine ya utangazaji.

Tukiangazia haki hizi katika Michezo ya Olimpiki, Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa (The International Olympic Committee) ilifanya juhudi kuhakikisha ulinzi wa haki hizi. Kwanza, Kamati hii ilianzisha kituo rasmi cha kutoa matangazo yote yanayohusisha michezo ya Olimpiki. Kituo hiki kinaitwa The Olympic Broadcasting Services (OBS). Kamati hii pia, inapatia OBS mamlaka ya kumiliki haki miliki za uchapishaji wa michezo ya Olimpiki.

Mamlaka kuu ya OBS ni kuchapisha na kutangaza michezo mbalimbali ya Olimpiki moja kwa moja kupita majukwaa yote ya utangazaji kama vile televisheni, redio, mitandao ya kidijitali na mengineo. Uchapishaji huu unalenga na unafaa kufikia mabilioni ya watazamaji wote ulimwenguni, haswa kwa sababu michezo ya Olimpiki huhusisha takriban nchi zote duniani. Hata hivyo, hili ni jukumu kubwa kwa stesheni moja na OBS inaweza kosa kufaulu kutimiza animio hili. Kwa hivyo na ili kuhakikisha habari za michezo kadhalika zinawafikia watazamaji wengi, OBS hushirikiana na mashirika mengine ya utangazaji, wanotambulika kama Rights Holding Broadcasters (RHBs). RHBs hupata haki za kipekee kutoka OBS kwa njia ya leseni/ruhusa spesheli. Hizi leseni huwapapa RHBs idhini ya kutangaza, kuchapisha na kupeperusha Michezoya Olimpiki nchini kwao na/aumaeneo mengine wanayokubalishwa na OBS.3

OBS, kama wenye haki hizi miliki za utangazaji, huangazia wajibu wa RHBs katika leseni zao. Leseni hizi pia hutoa maelezo ya jinsi haki husika zinafaa kutumika wakati wa kutangaza, kuchapisha na kupeperusha Michezo ya Olimpiki. Ukiukaji wa masharti yaliyopeanwa katika leseni ni sawa na kukiuka haki miliki za OBS, na OBS ina haki ya kutamatisha leseni hiyo.

Nchini Kenya, mwaka huu stesheni ya Standard Group lilipokea leseni kutoka OBS. Leseni hii iliwapa (Standard Group) idhini ya kipekee ya kupeperusha Michezo ya Olimpiki 2020, moja kwa moja kupitia stesheni yao ya Kenya Television Network (KTN). Kwa sababu leseni hii ilikuwa ya kipekee, vituo vingine vya utangazaji, kama vile NTV, havingepeperusha Michezo hii. Hata hivyo, hizi stesheni zingine hukubalishwa kutangaza mambo muhimu ya mchezo hii kama vile ushindi wa timu mbali mbali. Ubaguzi huu wa utangazaji wa mambo muhimu unakubalika na unabainishwa na sheria. Ubaguzi huu unaazimia kuipa michezo au kazi za ubunifu hii umuhimu wao katika jamii.

Zaidi ya kumpa mmiliki wake uwezo wakuamua jinsi kazi zao zitasambazwa na kuchapishwa, haki za utangazaji pia huwapa wanaozimiliki nafasi ya kupata faida za kiuchumi. Njia moja mashirika ya utangazaji hupata faida ni kupitia leseni. Leseni ni mkataba unaomruhusu mtu kumiliki au kutumia mali/kitu/kufanya jambo fulani. Hivyo basi, leseni ya haki za utangazaji mara nyingi huwapa mashirika na vituo vingine vya utangazaji ruhusa ya kusambaza na kuwasilisha kazi husika katika stesheni zao za utangazaji. Mara nyingi, wanaopokea leseni hizi hulipa wamiliki wa haki za utangazaji kama fidia ya kuwapa ruhusa ya kutumia na kusambaza kazi zao. Tukirejelea mfano wa Michezo ya Olimpiki, wanaotuzwa haki za kipekee za kuwasilisha michezo hulipa OBS ilikupokea siginalizinazohitajika kuwezesha usambazaji wa michezo hiyo moja kwa moja.

Isitoshe, mashirika ya utangazaji, sana sana yanayopeperusha hewani vipindi maarufu, pia hupata faida za kiuchumi kwa kuvutia mapato kutoka kwa kampuni na watu wanaotaka kutangaza biashara zao kwa umma (advertising revenue). Kwa mfano, Standard Group, kwa sababu ya kutuzwa haki ya kipekee ya kuwasilisha Michezo ya Olimpiki, lingetarajiwa kufaidika kifedha kwa kuwauzia makampuni nafasi za kuwatangazia na kuwaelezea umma kuhusu bidhaa na huduma zao.

Ni muhimu pia kukumbuka kuwa ukiukaji wa haki hizi huweza kusababisha kufunguliwa kwa mashtaka ama kesi kortini. Ukiukaji wa haki za utangazaji hutendeka pale ambapo vipindi husambazwa bila idhini na ruhusa ya mmiliki wa haki ya utangazaji wa kipindi husika.

Hitimisho

Kuwepo kwa haki za utangazaji na uwezo wa kuleseni haki hizo huruhusu na kuendeleza uwasilishaji na usambazaji wa habari. Pia huwapa mashirika ya utangazaji motisha ya kutaka kuunda au kuendelea kubuni kazi mpya na tofauti. Isitoshe, kuimarika kwa teknolojia utazidi kufafanua upya njia zingine za kutekeleza haki hizi.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked