ULINZI WA ALAMA ZA BIASHARA

  • Cynthia Nzuki
  • |  
  • November 11, 2020
  • |
  • Trademark
ULINZI WA ALAMA ZA BIASHARA

Chema cha jiuza, kibaya cha jitembeza.

Katika uandishi wa hapo awali tuliangalia jinsi kazi za kisanaa hulindwa. Uandishi wa leo utazingatia ulinzi wa alama za biashara.

Alama za biashara ni ishara, michoro au maandashi yanoyotambulisha bidhaa na huduma za biashara maalum. Mifano ni kama jina Coca-Cola, tunda linalotumika kwenye bidhaa za elektroniki za kampuni ya Apple, jina Safaricom na rangi ya kijani inayotumika na kampuni ya Safaricom. Alama hizi hulindwa na husajiliwa chini ya sheria ya Trademarks Act, CAP 506.

Kulingana na vifungu 12 na 13 vya Trademarks Act, ndiposa alama iweze kusajiliwa lazima iwe tofauti na ya kipekee. Hii ina maana kuwa lazima iweze kutofautisha bidhaa na huduma za biashara moja kutoka kwa zingine. Kingine cha muhimu ni kuwa alama zenyewe hazifai kutoa maelezo kuhusu bidhaa au huduma inayotambulishwa. Zaidi, kifungu cha 14 kinaamrisha kuwa alama zilizo na lengo la kuwa danganya na kuwa changanya wateja wa bidhaa na huduma, hazitasajiliwa.

Alama hizi za kutambulisha bidhaa na huduma mbali mbali husajiliwa Kenya Industrial Property Institute (KIPI); kulingana na maagizo yaliyomo katika Trademarks Act na Trademarks Rules. Isitoshe, alama hizi husajiliwa kwa heshima ya jinsi bidhaa na huduma huuainishwa. Uainishaji huwa kulingana na The Nice Classification.Usajili unapokamilika, mmliki wa alama iliyosajiliwa hupewa cheti cha kudhibitisha usajili na haki ya kutumia alama yake kwenye soko huru. Haki hizi pia huweza kupitishwa kutoka kwa mja mmoja hadi mwingine kwa njia ya leseni, kuuzwa au kwa kupeanwa.

Haki katika alama iliyosajiliwa hudumu kwa muda wa miaka kumi (10). Kulingana na kifungu cha 23 cha Trademarks Act, mmiliki anaweza ongezewa muda huu kwa miaka ingine kumi akilipa ada iliyowekwa na sheria.

Mara kwa mara haki hizi hukiukwa na watu bila ruhusa ya mmiliki wa haki hizo. Kulinganana sheria, ukiukaji huu ni hatia. Mkiukaji wa haki hizi ana weza kupelekwa kortini kujibu mashtaka.

Kwa upande mwingine, kunazo alama za biashara ambazo hazijasajiliwa. Wenye alama hizi wana uhuru wakuzitumia kwenye soko huru ili kutambulisha bidhaa na huduma zao; lakini kulingana na kifungu cha 5 katika Trademarks Act, hawana haki ya kurudishiwa hasara au fidia kutokana na ukiukwaji wa alama hizo.

Kutamatisha, kama mwana biashara, ni muhumu kujua kuwa kuna sheria ambayo inalinda jinsi unavyotambulisha bidhaa na huduma zako. Ni muhimu kuzisajili alama hizi kwani katika dunia ya biashara jina ndilo huuza.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked