ULINZI WA UVUMBUZI WA VYOMBO NA MICHAKATO BUNI
- Cynthia Nzuki |
- November 18, 2020 |
- Copyright,
- Intellectual Property,
- Patent,
- Trademark
Kidole kimoja hakivunji chawa.
Uandishi wa hapo awali ulizingatia jinsi alama za biashara husajiliwa na pia jinsi zinalindwa. Hapo mbeleni tuliangazia jinsi ya kulinda sanaa. Uandishi wa leo utaangazia ulinzi wa uvumbuzi wa vyombo na michakato buni; ambazo mara nyingi hutumika viwandani kurahisisha kazi.
Mfano ya chombo na mchakato buni ni kama mashine inayotumika kufua nguo. Uvumbuzi wa vyombo na michakato buni hulindwa na sheria ya Industrial Property Act, No. 3 of 2001.
Kulingana na kifungu cha 21, vyombo na michakato buni hueleweka kuwa sulihisho maalum kwenye uwanja wa teknolojia. Na kulingana na kifungu cha 22, ndiposa chombo au mchakato buni uweze kupata ulinzi, lazima uwe mpya, umechukua hatua ya uvumbuzi na uweze kutumika viwandani.
Kulingana na kifungu cha 23, kizingiti cha kuwa mpya huzingatia kama kuna ushahidi au maelezo yoyote, inayojulikana na watu wa umma, kuhusu chombo au mchakato unaotaka kusajiliwa. Kama ipo, chombo hicho au mchakato huo buni si mpya.
Hatua ya uvumbizi, kulingana na kigungu cha 24, ina maana kuwa kilicho buni, na kinachotaka kusajiliwa, hakifai kuwa dhahiri. Hii ina maana kuwa, chombo au mchakato buni haufai kutarajiwa na mtu mwenye ujuzi katika uwanja au sekta ya uvumbuzi huo.
Kizingiti cha kuwa na uwezo wa kutumika viwandani inahitaji kilicho buni kiwe na asili ya kutumika katika kiwanda moja au kingine.
Usajili wa uvumbuzi wa vyombo na michakato buni hutekelezwa na Serikali kupitia Kenya Industrial Property Intitute (KIPI). Usajili unafuata sheria iliyowekwa na Industrial Property Act(IPA) na Industrial Property Tribunal Rules, 2002. Kulingana na kifungu cha 30 cha Industrial Property Act, mvumbuzi ana haki ya kupata ulinzi dhidi ya uvumbuzi wake. Kufuatia kifungu 33, jina la mvumbuzi lazima litajwe kwenye fomu za kuomba usajili, isipokuwa pale ambapo hataki litajwe. Kufuatia kifungu cha pili, mvumbuzi lazima awe mtu au watu sio kampuni.
Usajili unapokamilika, mmliki hupewa cheti cha kudhibitisha usajili na haki yake. Kulingana na kifungu cha 53, mvumbuzi anaweza kutumia au kuzuia matumizi ya uvumbuzi wake atakavyo.
Haki katika uvumbuzi uliyosajiliwa hudumu kwa muda wa miaka ishirini (20) kutoka tarehe ya kufungua ombi la usajili. Baada ya muda huu, maelezo yote kuhusu chombo au mchakato uliolindwa huwa mali ya umma na unaweza tumiwa na mtu yeyote bila ruhusa ya mvumbuzi. Juu ya haya, kila mwaka, mmliki wa haki hizi za uvumbuzi anapaswa kulipa ada. Kwa kulipa hii ada, mvumbuzi huashiria ya kwamba anatumia uvumbuzi wake kiwandani au kwa manufaa ya viwanda nchini. Haki hizi pia huweza kupitishwa kutoka kwa mja mmoja hadi mwingine kwa njia ya leseni, au mkataba.
Haki hizi zinaweza kukiukwa na yeyote anayetumia uvumbuzi au mchakato uliosajiliwa bila ruhusa ya mmiliki. Kulingana na sheria, ukiukaji huu ni hatia na kifungu cha 55 kinampa mmiliki ruhusa ya kutekeleza na kulinda haki zake. Hivyo basi, mkiukaji wa haki hizi anaweza kupelekwa kortini kujibu mashtaka na kumplipa fidia mmiliki. Pia korti linaweza amrisha mkiukaji akome ukiukaji huo.
Kama nilivyoashiria hapo awali, ni muhimu kulinda na kusajili kazi zako buni na zilizotokana na mawazo yako. Usajili wa haki miliki una uhusiano mkubwa sana na ukuaji wa uchumi wa nchi yetu. Hivyo basi, ni himizo kwetu kulinda haki miliki kila wakati.